KAMANDA wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amewaagiza askari kuhakikisha wanampata akiwa hai au amekufa mhalifu aliyetekeleza mauaji ya kinyama ya askari wa kikosi cha usalama barabarani, Sajini Mensah Ponda Dishe.
Aidha, amesema hata kama mtu aliyefanya unyama huo yuko ndani ya familia, jeshi hilo litahakikisha linamshughulikia ipasavyo ili haki ipatikane.
Aliyasema hayo jana wakati akiongoza mamia ya askari na wananchi waliojitokeza kuuaga mwili wa askari huyo katika viwanja vya nyumba za polisi Kunduchi. “…Nimewaambia askari walio chini yangu wafanye kila liwezekanalo ili mhalifu aliyehusika kufanya tukio hili la kinyama akamatwe akiwa mzima au akamatwe akiwa amekufa ili haki itendeke,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema hata kama mhalifu huyo atabainika kuwa yuko ndani ya familia ya askari huyo, Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua za kisheria ili kuhakikisha haki imepatikana.
Kamanda Sirro alisema, alipopata taarifa za askari huyo kupigwa risasi alikwenda hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini aliambiwa kuwa amepelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambapo alipofika aliambiwa kuwa ameshapoteza maisha kwa kuwa alipigwa risasi kwa karibu sana.
Alisisitiza askari wote kuhakikisha wanatenda haki, wanakataa rushwa ili hata siku ya mwisho wakati wa hukumu ya Mwenyezi Mungu waweze kwenda sehemu salama.
Post a Comment