Loading...

Breaking News: HILI NDILO TAMKO ZITO LILILOTOLEWA NA TUME YA VYUO VIKUU (TCU) NA NACTE JANA, SERIKALI HII KIBOKO

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Bi. Maimuna Tarishi ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)   kufuta programu zinazotolewa na vyuo vikuu hapa nchini ambazo hazijafanyiwa tathmini wala kusajiliwa.

Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga maonyesho ya kumi na moja ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoanza Julai 20 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Wakati mwingine najiuliza inakuwaje chuo kinafundisha programu ambayo haijatathminiwa wala kusajiliwa na TCU au NACTE, ni lazima tuwe makini kwani tunahitaji elimu bora katika vyuo vyote nchini bila kuangalia kama ni cha Serikali au ni Binafsi,” alifafanua Bi. Tarishi.

Aliendelea kwa kusema kuwa, TCU na NACTE wanajukumu ya kuzifuta programu hizo na kuanzisha programu zenye uhitaji mkubwa kama vile shahada ya mafuta na gesi, Kompyuta na Ualimu wa Sayansi ambapo wataalamu katika maeneo hayo wamekuwa wakihitajika zaidi katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inajikita zaidi katika uanzishwaji wa viwanda.

Aidha Bi. Tarishi amewataka TCU na NACTE kudahili wanafunzi wenye vigezo vinavyohitajika na kusisitiza kuwa ni bora kuwa na wanafunzi wachache katika vyuo vikuu kuliko kuwa na wanafunzi wengi ambao hawana sifa.

Wakati huo huo Mkuu wa Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Zanzibar Salehe Mwinyi amesema kuwa wanafunzi wengi wamejitokeza kutembelea banda la Chuo hicho kutaka kujua pogramu zinazotolewa na wengi wao wameonyesha nia ya kujiunga katika Chuo hiko.

Vile vile Mwinyi amesema kuwa mwaka huu idadi ya wanafunzi waliotembelea maonyesho hayo ni wengi zaidi kutokana na eneo lililochaguliwa kufikika kwa urahisi kutoka pande zote za jiji la Dar es Salaam ukilinganisha na mwaka jana ambapo yalifanyika viwanja vya Saba Saba na kutembelewa na idadi ndogo ya wanafunzi na wazazi.

Kwa upande wake, Fadia Suleiman mwanafunzi anayetegemea kujiunga na Chuo Kikuu mwaka huu, amesema kuwa maonyesho hayo yamemsaidia kwa kiasi kikubwa kujua ni programu gani asome kutokana na ufaulu wake wa kidato sita.

Maonyesho ya  Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambayo huandaliwa na TCU hufanyika kila mwaka yakitoa fursa kwa Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya nchi kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi wanaotegemea kujiunga na vyuo vikuu kwa mwaka husika juu ya programu zinazotolewa na vyuo hivyo pamoja na kutoa ushauri ni programu gani mwanafunzi asome kwa kuangalia ufaulu wake.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright BAKI NASI | Designed By BAKI NASI
Back To Top