Maazimio hayo ambayo yanaitwa ‘mazito na makubwa’ kuwahi kutolewa na chama hicho katika siku za hivi karibuni, yanatarajiwa kuonyeshwa moja kwa moja na vituo vitatu vya runinga nchini.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya chama hicho kimeeleza kuwa maazimio hayo ya Kamati Kuu yatatangazwa moja kwa moja kupitia baadhi ya vituo vya runinga kutoa fursa kwa Watanzania kusikiliza maazimio hayo.
Kamati kuu ya Chadema imefanya kikao chake kwa siku nne mfululizo kikiwa kimeghubikwa na usiri mkubwa.
Taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari jana, ilisema Kamati Kuu ilimaliza kikao chake cha siku nne jana na leo maazimio yake yatawekwa wazi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema kupitia mkutano huo yatatangazwa maazimio ya kikao hicho kilichohitimishwa Dar es Salaam jana.
Taarifa hiyo ilisema Chadema kitatoa tamko zito la ukubwa wa aina yake.
“Licha ya mambo hayo chama kitatoa matamko mazito na makubwa ya aina yake ambayo hayajawahi kutolewa na chama chetu katika siku za karibuni."
Taarifa hiyo ilisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya kina juu ya masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ya siasa nchini kwa sasa ambayo inatishia hali ya uchumi na ustawi wa jamii nzima kwa ujumla, hivyo taifa zima kuwa katika majaribu makubwa ya kukosa mwelekeo wa uongozi.
“Kupitia mkutano huo, Chadema kitatoa mwelekeo wa hali ya nchi hasa wakati huu ambao taifa linaonekana kukosa dira ya uongozi kwa ajili ya ustawi wa Watanzania wote kwa ujumla” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kuwekwa wazi jina lake.
“Kupitia mkutano huo, chama kitazungumzia mipango ya kujiimarisha kuendelea kuwatumikia wananchi na kusimamia dira ya mabadiliko na uhuru wa kweli nchini,”alisema Makene.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Makene alisema suala hilo halijathibitishwa rasmi kama mkutano huo utaonyeshwa moja kwa moja katika runinga.
“Hata mahali utakapofanyika mkutano huo bado hapajajulikana, nitakupigia simu kesho asubuhi (leo) kukujulisha wapi tamko hilo litatolewa." Alisema
Post a Comment