TAARIFA YA MRADI WA MACHINGA COMPLEX
1.0 Utangulizi
Mnamo tarehe 19 Aprili, 2016 ofisi yangu ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ilipokea barua ya agizo la waziri wa nchi TAMISEMI juu ya kusimamia uendeshaji wa mradi wa Machinga Complex. Ambapo katika kutekeleza agizo hilo nilichukua hatua ya kwanza na ya muhimu ya kuupitia mkataba wote wa mradi huu ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya haki na wajibu wa pande mbili zilizohusika kwa maana ya Halmashauri ya Jiji na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Kimsingi, tathmini yangu ya mkataba ililenga kubainisha na kujiridhisha juu ya mambo sita yafuatayo; aina ya jengo lililotarajiwa kujengwa, usimamizi wa fedha za mkopo, usimamizi wa ujenzi wa mradi, gharama za mradi, utaratibu wa urejeshaji wa deni na kiwango cha riba kilichoainishwa. Ikukumbukwe tu kwamba, wakati halmashauri ya jiji ikikabidhiwa mradi siku ya kwanza ilikuwa tayari inadaiwa kiasi cha bilioni 19.7 huku mpaka Machi mwaka huu deni lilishafikia kiasi cha bilioni 38 za kitanzania, kutokea kwenye mkopo wa bilioni 12.7
2.0 Uchunguzi
Baada ya kupitia kwa umakini mkataba mzima na kukagua mradi wenyewe, zoezi ambalo lilihusisha kulinganisha kati ya kilichofanyika baada ya mradi kukamilika na taarifa ya upembuzi yakinifu (feasibility study) uliofanyika kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi nimebaini yafuatayo;-
2.1 Ukubwa halisi wa jengo
Nimebaini kwamba majengo ya sasa ya machinga complex hayakujengwa kwa ukubwa sawa na ule ambao Halmashauri ya Jiji na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) walikubaliana kwenye mkataba na kupitia kifungu cha 1.1 cha barua ya makabidhiano kinachoeleza kwamba jengo lililokabidhiwa lina sehemu yenye ghorofa 5 na ghorofa 6 ili liweze kumudu idadi ya machinga wasiopungua 10,000 wakati hali halisi baada ya kutembelea jengo hilo ni kwamba jengo lina ghorofa 4 zinazobeba machinga 4,000 tu. Kwahiyo, pamoja na kwamba barua ya makabidhiano ilisainiwa na pande zote mbili licha ya ukweli kuwa maelezo ya jengo yalikuwa tofauti na jengo lenyewe.
2.2 Usimamizi wa fedha za Mkopo
Kwenye usimamizi wa fedha za Mkopo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye ni mkopaji hakuhusika na usimamizi wa fedha za mkopo, hivyo mkopeshaji hakuwa na udhibitisho wa gharama halisi, jambo ambalo si tu limefanya mkopaji kutojua gharama halisi za jengo bali pia kulipokea likiwa limechelewa na likiwa halina ukubwa ulioelezwa kwenye mkataba. Kimsingi, haya yote yanazaliwa na maelekezo ya kifungu namba 4.1 kinachoeleza kwamba, mkopeshaji kusimamia mradi kuanzia hatua ya usanifu hadi kukamilika kwake ikiwa ni pamoja na kufanya malipo moja kwa moja kwa mkandarasi na mshauri wa mradi, kwa maneno mengine pia ni kwamba kifungu hiki kinakinzana na vifungu namba 2.1, 2.2, 10.1 na 11.1 vya mkataba huohuo ambavyo vinaelekeza kwamba mkopeshaji (NSSF) atatakiwa kutoa fedha kwa mkopaji (Halmashauri ya Jiji) kwa ajili ya kugharamia mradi pekee na kuusimamia kama ulivyokubalika kwenye mkataba.
2.3 Kuhusu gharama za mradi
Nimebaini kuwa fedha za mkopo ziliongezeka toka shilingi bilioni 12.14 za kwenye mkataba na kufikia bilioni 12.7 ikiwa ni nyongeza ya shilingi milioni 560, nyongeza ambayo ilifanyika bila makubaliano yoyote kati ya mkopeshaji na mkopaji, hali ambayo haimtendei haki mkopaji. Kwa faida tu ya wanadar es salaam na watanzania wenzangu ni kwamba, halmashauri ya jiji ilitiliana saini ya makubaliano na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) ya mkataba ambao unalenga kuipatia halmashauri ya jiji mkopo wa bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu ingawa baada ya muda kidogo mkopeshaji (NSSF) alisema kuwa bilioni 10 na hivyo kufanya marekebisho ya mkataba na kuongeza mkopo wa bilioni 2.14
2.4 Urejeshaji wa deni
Suala la urejeshaji wa mkopo unazua utata pale mkataba unapoainisha kuwa, mkopaji ataanza kulipa marejesho ya deni kuanzia tarehe 31 Desemba, 2008 tarehe ambayo mradi ulikuwa unatarajiwa kuwa tayari umeanza lakini mkopeshaji (NSSF) alikuwa hajamaliza ujenzi, na cha ajabu mkopaji (Halmashauri ya Jiji) alitakiwa kuanza kulipa deni hata kabla ya muda wa grace period kuisha wakati jengo likiwa bado lipo mikononi mwa mkopeshaji ambaye alijitwisha jukumu la ujenzi huku akiwa bado akang’ang’ania kulipwa riba.
mara tu tarehe hiyo ilipofika hata kama mpokeshaji mwenyewe alikuwa bado hajakamilisha ujenzi huku akidai pesa ya riba.
Uwezo wa Mradi
Uwezo wa jengo hilo lililopo hata kama litafanya kazi kwa uwezo wake wote kwa maana ya kujaza nafasi zote zilizopo ni kasi cha sh124,796,666.666 kwa mwezi ambazo ni sawa na kiasi cha sh1,497,560,000 kwa mwaka. Pungufu ya 60% ya lengo la Mradi kama ilivyokuwa kwenye upembuzi yakinifu
3.0 Mapendekezo
3.1 Baada ya uchunguzi huu ulionifanya kuamini mambo makubwa matano niliyoyaainisha hapo chini na ambayo yameniongoza kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua;-
- Deni halilipiki – ukweli ni kwamba, ukizingatia kiasi cha pesa kinachodaiwa kutoka kwa halmashauri ya Jiji ambacho mpaka sasa ni zaidi ya bilioni 38 utagundua kuwa, halmashauri haiwezi kulipa deni hilo. Ikilinganishwa na uwezo wa jengo hilo deni hili litalipwa baada ya miaka isiyopungua 24
- Mkataba wote huu ni wa hovyo na haukupaswa kusainiwa hata kidogo.
- Kitendo cha kusaini mkataba huu ni hakika na bayana kuwa rushwa ilitumika pande zote mbili, kwa maana haiwezekani ukaacha taaluma yako kwa kiwango hicho cha kutoona udhaifu huu wa wazi wa mkataba huu kama hujapofushwa macho na rushwa.
- Mkataba huu hauna tija kwa upande wowote ule: sio NSSF kwasababu halmashauri ya Jiji hawana uwezo wa kulipa deni, wala sio kwa Jiji lenyewe kwani halina uwezo wa kutekeleza mkataba kwa kufanya malipo yanayotakiwa na hauna faida vilevile kwa machinga kwa sababu gharama ya kupanga ni kubwa.
3.2 Mapendekezo
- Kuvunjwa kwa mkataba na NSSF kuchukua eneo lao, kwa makubalino ya kwamba, Halmashauri ya Jiji walipwe kodi ya ardhi jambo ambalo linaweza kufanyika kwa urahisi kupitia NSSF na halmashauri ya Jiji kumiliki hisa kwa pamoja.
- Au NSSF wakabidhi jengo kwa halmashauri ya Jiji, lakini wakae na kukubaliana upya na hivyo kuandika mkataba tofauti na ule wa mwanzo.
- Mwisho, wahusika wote wa pande zote mbili wachukuliwe hatua kwani hatuwezi kutumia fedha za mifuko za hifadhi ya jamii ambazo ni fedha za wanyonge wa taifa hili kwa faida ya wachache waliotanguliza ubinafsi,.
Imetolewa na:
Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa – Dar es Salaam.
1 comments:
thumb up makonda wewe ni aina ya kiongozi ambaye nchi sasa inahitaji
ReplyPost a Comment