Loading...

HAPATOSHI TENA BAADA YA SERIKALI KUTOA KAULI YA KUHAKIKI VYETI KWA WANACHUO WOTE NA WAFANYAKAZI, WANASHERIA WATOA TAMKO KALI SANA

SIKU mbili baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, kutangaza mchakato wa kufuatilia wahitimu wa vyuo vikuu walioingia bila kuwa na sifa, wanasheria wametofautiana juu ya hatua hiyo.
 Prof. Ndalichako alisema juzi kuwa, serikali itahakiki na kisha kufuta udahili wa wanafunzi walio katika vyuo vikuu, ambao walijiunga bila ya kuwa na sifa.
Baadhi ya wanasheria hao wamesema suala hilo haliwezekani kwani vyuo vilivyosomesha wanafunzi hao ndiyo vinapaswa kuchukuliwa hatua, lakini wengine wamesema suala hili liko wazi kisheria, kwani mtu akighushi vyeti anakuwa amefanya kosa la jinai.
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola, alisema suala la kufutiwa vyeti kwa wahitimu walioingia chuoni kiujanjaujanja haliwezekani kwa kuwa wanafunzi hao walisoma na kumaliza kwenye vyuo husika.
Alisema uzembe umefanyika kwenye vyuo vilivyowapokea wakati wakijua wanafunzi hao hawana sifa.

“Hapo wenye makosa ni vyuo vilivyowaruhusu kuendelea kusoma hadi kuwapatia vyeti, haiwezekani mwanafunzi asiye na sifa ukamuachia akasoma, anaanza mwaka wa kwanza, mwaka wa pili na wa tatu halafu anamaliza unampatia cheti eti umfutie cheti chake wakati mitihani alifanya na kufaulu,” aliongeza Stola.
Alitolea mfano wa mtu akivamia ardhi halafu akaachwa bila ya kuondolewa, sheria inampa mvamizi haki ya kumiliki ardhi.
Stola alisema vyuo vilivyowapokea wanafunzi hao vinatakiwa kulaumiwa pamoja na ngazi za juu kwa kuruhusu kutokea kwa uzembe huo.
Hata hivyo, mwanasheria mwingine, Prof. Abdallah Safari, ametoa kauli inayopingana na ile ya Stola, akisema kisheria suala hilo lipo wazi, kama mtu ameghushi vyeti hatua za kisheria zinatakiwa kuchukuliwa ikiwemo kunyang’anywa cheti hicho.
Alisema changamoto iliyopo ipo kwenye mfumo uliopo wa kuruhusu mambo hayo kujitokeza.
“Mfumo wetu wa nchi unatoa mwanya kwa watu kughushi vyeti, katika hali ya kawaida inatokea vipi wanafunzi wanaingia chuoni kiujanjanja, tusichezee sekta ya elimu,” alisema Prof. Safari.
Aliongezea kuwa, katika nchi za Ulaya mtu akibainika ameghushi cheti, basi chuo kina halali ya kukunyang’anya cheti kilichotoa.
Alisema hapa nchini suala la elimu bora halizingatiwi na ndio maana limeathiri sekta nyingi.
“Mfano kwenye mahakama kuna changamoto, kuna hukumu zinatolewa hadi unajiuliza huyu sheria kasomea wapi, ndiyo maana namuunga mkono Mbunge Tundu Lissu alivyolalamikia masuala ya majaji na pia ipo hatari ya nchi kuwa madaktari wasio na sifa na kutuchezea afya zetu,” alionya Prof. Safari.
Mwanasheria mwingine, Denis Maringo, alisema kufutiwa vyeti hivyo kisheria inawezekana, lakini inapaswa kufuata taratibu na misingi ya kisheria.
“Inawezekana kwa sababu kwa kawaida kama kweli vyeti husika vilighushiwa ama wahusika walipata shahada zao baada ya kuingia vyuo vikuu kwa vyeti ambavyo havikuwa halali kule sekondari, basi vyeti ama shahada wanazozipata kutoka vyuo vikuu vinakuwa batili,” alisema Maringo.
Alisema vinakuwa batili kwa sababu kisheria kuna nadharia inayosema kwamba, huwezi ukapata uhalali kutokana na kitu ambacho kilikuwa batili awali.
“Hii inatokana na msemo wa kisheria usemao kitu kilichokuwa batili kutoka mwanzo ni batili, mfano halisi huwezi ukapata kifaranga kutoka katika yai lililoharibika,” aliongeza Maringo.
Maringo alisema kisheria lazima wahusika hao kupatiwa nafasi ya kujitetea na kwa kufuata taratibu na kanuni za haki za kiasili .
Mwanasheria mwingine, Jacob Mogendi, alisema kitendo cha kujiunga chuoni kwa kughushi vyeti kwa mujibu wa sheria ni kosa na unaweza kufungwa ama kutakiwa kulipa faini.
Alisema kabla ya kuanza kusoma kuna makubaliano ambayo mwanafunzi anatatakiwa kuingia na chuo kwa kuhakikisha taarifa alizoziwasilisha zipo sahihi na mkataba unaeleza kama hazitakuwa sahihi atachukuliwa hatua.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright BAKI NASI | Designed By BAKI NASI
Back To Top