Ndivyo hali ilivyo sasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako anasubiri kukabidhiwa kofi ya uenyekiti na kufanya mabadiliko, ambayo yanatazamiwa kuanzia kwa wajumbe 14 wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Mwenyekiti wa sasa wa CCM, Jakaya Kikwete, ataendeleza utamaduni uliozoeleka ndani ya chama hicho, kuwa pale mtu anapong’atuka urais wa nchi basi anakabidhi uongozi wa chama kwa mrithi wake.
Rais Magufuli ambaye alimrithi Kikwete baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, anatazamiwa kuanza kupanga timu yake mara moja kwa kuanzia na Kamati Kuu ya CCM (CC) baada ya kukabidhiwa kofia ya uenyekiti kwenye mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika kesho mjini Dodoma.
Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, aliiambia Nipashe jana kuwa, kazi ya kwanza ya Rais Magufuli baada ya kukabidhiwa uongozi wa CCM itakuwa kuunda sekretarieti ya kumsaidia baada ya kupata baraka za Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Alisema NEC inatarajia kukutana keshokutwa Jumapili, lakini kwa kutegemeana na utashi wa mwenyekiti mpya.
Ole Sendeka alisema NEC ikikutana ndiyo itatoa ridhaa ya kuachia ngazi kwa sekretarieti iliyokuwa inamsaidia mwenyekiti anayeng’atuka na kuridhia kusukwa upya kwa sekretarieti hiyo.
“Kama kuna mabadiliko anataka kufanya kwenye safu za uongozi wa chama itahitajika ridhaa ya NEC, ambayo mwenyekiti mpya, Rais Magufuli ndio mwenye uamuzi wa kuitisha kikao chake,” aliongeza Ole Sendeka.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ametangaza ataachia ngazi pamoja na Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye.
Baadhi ya makada wa CCM, wamelidokeza Nipashe mjini hapa kuwa, mabadiliko ndani ya Kamati Kuu na ngazi nyingine za uongozi wa chama hicho yatatokana na tathmini ya Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho.
Kamati hiyo ambayo pia mwaka jana ilitumika kukata vigogo wa chama hicho waliokuwa wanawania kuipeperusha bendera ya CCM kwenye urais, ubunge na udiwani, inaelezwa ilitarajiwa kufanya tathimini ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana kuanzia wakati wa kura za maoni na hali ya sasa ya kisiasa nchini.
Kamati hiyo ambayo kawaida hukutana kwa siri, inaelezwa pia kuwa ilitazamiwa kupitia majina ya watu wanaodaiwa kusaliti chama wakati wa Uchaguzi Mkuu na kumuunga mkono aliyekuwa mgombea urais aliyepeperusha bendera ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.
Lowassa alitikisa ulingo wa siasa nchini baada ya kuihama CCM Julai mwaka jana kufuatia jina lake kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Tayari vikao mbalimbali vya CCM kuanzia ngazi ya wilaya vimefanyika na kuna baadhi ya watu wamesimamishwa kutokana na tuhuma hizo, huku wengine wakikata rufaa kwenye ngazi za juu.
Sasa kama ambavyo matokeo ya kamati hiyo ya maadili na usalama yaliliza vigogo wengi wa CCM, akiwamo aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali, aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Lowassa, inategemewa kutikisa wengine wengi baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa chama na ripoti ya kamati hiyo.
UTARATIBU ULIVYO
Kwa utamaduni wa CCM, Mwenyekiti wa CCM hutakiwa kuwasilisha majina 14 ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na idadi kama hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Wajumbe wa NEC hutakiwa kuchagua wajumbe saba kutoka katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa utaratibu huo wajumbe 14 wa Kamati Kuu wapo roho juu kutokana na kutojua hatma hayo kama watarudi au watang’olewa kufuatana na utashi wa mwenyekiti mpya.
WALIOKALIA KUTI KAVU
Kwa sasa wajumbe wa CC ambao wanatokana na mwenyekiti anayemaliza muda wake, kwa Tanzania Bara ni Stephen Wasira, Pindi Chana, Prof. Anna Tibaijuka, Jerry Silaa, Adam Kimbisa, Dk. Emmanuel Nchimbi na William Lukuvi.
Wajumbe hawa wako kwenye hatihati kuteuliwa na Magufuli na sababu kubwa ni kutokana na makundi ya uchaguzi mkuu ambao baadhi yao walipinga waziwazi kuenguliwa kwa wagombea waliowaunga mkono kuwania urais kupitia chama hicho, huku waliokatwa wakilia kuonewa.
Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe wa CC ambao ni chaguo la Kikwete walikuwa ni Vuai Nahodha, Hussein Mwinyi, Prof.
Makame Mbarawa, Dk. Salim Ahmed Salim, Maua Daftari, Hadija Aboud na Samia Suluhu, ambaye sasa ni mjumbe wa kamati hiyo kwa wadhifa wake wa Makamu wa Rais.
Sehemu kubwa pia ya wajumbe hawa inaweza isirudi kwenye nafasi zao kutokana na staili ya Rais Magufuli ya kupenda kutumia zaidi damu mpya.
Hata hivyo, kuna wakongwe waliotumikia chama hicho kwa muda mrefu bila shaka wataachia ngazi ili kupisha vijana.
WATAKAOBAKIA
Kwa upande wa wajumbe wa CC ambao watabakia kutoka na nyadhifa zao ni pamoja na Rais wa Zanzibar , Dk Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Idd Ali, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid.
Wengine ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Sadifa Juma, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee, Abdalla Bulembo na Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rwekiza.
Hata hivyo, angalizo kwa wajumbe wa CC kupitia jumuiya ni kuwa mwenyekiti anapewa nguvu na katiba ya chama hicho kuvunja uongozi wa jumuiya hizo na kuitisha uchaguzi wake, jambo ambalo linaweza kuwafanya kukosa sifa endapo watashindwa kutetea nafasi zao.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ambao wanatokana na kuwa wajumbe wa sekretarieti mbali ni Kinana na Nape, ambao wataachia ngazi, waliobakia watakuwa wanasubiri utashi na ridhaa ya mwenyekiti mpya na NEC nao ni, Naibu Katibu Mkuu-Bara, Rajabu Luhwavi, Naibu Katibu- Zanzibar, Vuai Ally Vuai, Katibu wa Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatib, Katibu wa Uchumi na Fedha, Zakia Meghji pamoja na Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Pindi Chana.
Post a Comment