Loading...
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam linawashikilia watu 1,065 kwa makosa mbalimbali ikiwemo
unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi kutoka maungoni na wapigabede.
Wamo pia watengenezaji na wanywaji wa pombe haramu aina ya gongo lita 952, mitambo mitatu, wavuta bangi na wachezaji kamari.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro alisema
kuwa watu hao walikamatwa maeneo tofauti ya jiji hilo.
Hata hivyo, askari walifanikiwa
kukamata silaha aina ya gobori Julai 21 mwaka huu maeneo ya Kawe,
Jangwani Sea Breeze. Hatua hiyo imekuja baada ya msako wa kuwatafuta
watuhumiwa sugu wanaotumia silaha za moto na kufanikiwa kukamata silaha
hiyo yenye namba HD 201-2014 ikiwa imetelekezwa maeneo hayo na watu
wasiofahamika.
“Silaha hiyo ilipatikana baada ya
askari kupata taarifa kutoka kwa raia kwamba kuna mtu wanamhisi ana
silaha na walipofika walikuta imetelekezwa kwenye eneo hilo. Msako wa
kuwatafuta watuhumiwa unaendelea,” alisema Sirro.
Alisema pia Julai 19, mwaka huu
walifanikiwa kukamata lita 952 za gongo maeneo mbalimbali na kati ya
lita hizo, lita 420 zilikamatwa Kinzudi Wazo Hill na kukamatwa
watuhumiwa sita na mitambo mitatu ya gongo na sukari kilo 100.
Wakati huo huo, kikosi cha usalama
barabarani kanda hiyo, kimekusanya zaidi ya Sh milioni 562.8 kutokana na
makosa mbalimbali. Sirro alisema idadi ya magari yaliyokamatwa ni
17,349, pikipiki 1,413, daladala 7,220, magari binafsi na malori 10,129.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, madereva
bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu
(helmet) ni 49 na jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 18,762. “Ukamataji
huu ni kuanzia Julai 15 mwaka huu hadi Julai 21 mwaka huu,” alisema
Kamanda Sirro.
Post a Comment